Wavu Taifa ni tambo tupu

0
10
WAKATI michuano ya Mabingwa wa Mikoa kwa Mchezo wa Wavu yakianza kwa kasi tangu juzi Alhamisi jijini hapa, makocha wa timu hizo wameanza tambo huku kila mmoja akidai ataondoka na taji.
Mashindano hayo yanashirikisha timu nane kutoka Mikoa mitano ya Tanzania Bara na Zanzibar, ambazo ni MTC, SAUT na Magu (Mwanza), Polisi na Nyuki (Zanzibar), Ngorongoro (Arusha) na SVC ya mkoani Shinyanga.
Wakizungumza na gazeti hili, baadhi ya makocha wa timu hizo, kila mmoja alijinasibu kutwaa ubingwa kutokana na ubora wa kikosi chake.
Kocha wa Polisi ya Zanzibar, Burhan Ally alisema haoni timu yoyote ya kuzuia kasi yao na wamekuja kwa nia moja tu kunyakua ubingwa.
“Tayari tumeanza na ushindi mnono wa seti 3-0 dhidi ya MTC na nia yetu ni kuendeleza ubabe hadi fainali na hatimaye kunyakua ubingwa,” alisema Ally.
Kwa upande wake, Kocha wa MTC ya Mwanza, Safari Yabunika alisema licha ya kuanza vibaya michuano hiyo, anaamini mechi mbili zilizobaki kwenye kundi lao atashinda.
“Tumepoteza leo (juzi) lakini tunajipanga na mechi zilizobaki dhidi ya SVC na SAUT kuhakikisha tunashinda na matarajio yetu ni ubingwa,” alisema Yabunika.
Naye Kocha wa SAUT, Teddy Peter alisema wanaenda kusahihisha makosa waliyoyafanya ili kurudi kwa nguvu kwenye michezo iliyobaki na kwamba ubingwa upo pale pale.
Mratibu wa mashindano hayo, Majaliwa Mayunga alisema kuwa kutokana na ushindani uliopo kwenye mashindano hayo, wanaamini watampata bingwa halali na mwenye uwezo.
Chanzo:Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here