Wapinzani Wa Yanga Caf, Wachanga Wanaojua

0
8
KUELEKEA kufuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika, Yanga imepangwa kucheza na Wolayta Dicha FC ya Ethiopia ambayo baadhi ya mashabiki wanadhani ni timu kibonde.
Wolayta ambayo pia inafahamika kama Wolaitta Dicha FC au Wolaitta Dicha SC si timu kongwe sana kwani ilianzishwa mwaka 2009 huko Wolayta Soddo na Chama cha Maendeleo cha Welayta.

Ni klabu mwanachama wa Shirikisho la Soka la Ethiopia, wakishiriki Ligi Kuu ya Ethiopia kuanzia msimu wa 2013/2014 huku mchezaji wake maarufu Mubarek Shikur, akiwa na timu hiyo tangu ilipoanzishwa mwaka 2009.
HAIJAWAHI KUTWAA UBINGWA WA LIGI
Tofauti na Yanga iliyotwaa ubingwa wa Ligi Kuu Bara zaidi ya mara 20, Wolayta wao hawajawahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Ethiopia zaidi ya mwaka jana kutwaa ubingwa wa Kombe la Ethiopia yaani Kombe la FA.
Ubingwa wao huo wa Kombe la FA ndiyo uliowapa nafasi ya kushiriki michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika mwaka huu ambalo linasimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).

ILIDHARAULIWA, IKAITOA ZAMALEK
Hadi inafika kucheza hatua ya kuwania kufuzu makundi ya Kombe la Shirikisho, Wolayta ilianza kwa kuitoa Zimamoto ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 2-1, kwani awali walipoenda Zanzibar walitoka sare ya bao 1-1 halafu nyumbani wakashinda bao 1-0.

Baada ya kuitoa Zimamoto, wakacheza na Zamalek ya Misri ambayo katika mechi ya kwanza wakicheza nyumbani Awassa kwenye Uwanja wa Wolayta Sodo walishinda mabao 2-1.
Ushindi huo uliwasha-ngaza watu wengi wa nje ya Ethiopia wakidhani Wolayta ni timu nyepesi, lakini hata katika marudiano timu hiyo ilifungwa mabao 2-1 na Zamalek na kuamuriwa kupigiana penalti.
Hata penalti zilipopigwa, Wolayta ikashinda kwa penalti 4-3 na kusonga hatua ya sasa ya mtoano ambapo timu za Kombe la Shirikisho zimechanganywa na zile zilizotolewa katika Ligi ya Mabingwa ikiwemo Yanga ili kucheza mechi za mtoano kutinga hatua ya makundi.
PASI ZAO NDIYO HATARI
Sifa kubwa ya Wolayta ni mchezo wao wa pasi nyingi huku wakitumia zaidi mfumo wa 4-3-3 jambo linalowapa nguvu ya kuzuia na kushambulia kwa wakati mmoja.
Katika mchezo wao dhidi ya Zamalek, pasi zao ziliwashangaza wengi kiasi cha kuonekana kuwa ni timu iliyojipanga kufanya kitu fulani katika msimu huu wa Kombe la Shirikisho Afrika.
Hii inawafanya Yanga kutakiwa kujiandaa kukabiliana na Wolayta ambayo inagonga pasi pengine kuliko Township Rollers FC ya Botswana ambayo iliitoa Yanga katika Ligi ya Mabingwa Afrika.
ZITAANZIA DAR
Mechi ya kwanza ya Yanga na Wolayta itachezwa kati ya Aprili 6 hadi 8, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwenye Uwanja wa Taifa, halafu zitarudiana kati ya Aprili 16 hadi 18, mwaka huu.
Chanzo: Global Publishers

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here