Wamekaa benchi na mabao yao England

0
4

LONDON, ENGLAND
LIGI Kuu England bado inaendelea kuwa ligi ya ushindani zaidi duniani. Ushindi umekuwa mkali zaidi ndani ya misimu miwili ya hivi karibuni baada ya ujio wa makocha matata kabisa kwenye ligi hiyo.
Makocha hao ni pamoja na Jurgen Klopp aliyetua Liverpool, Pep Guardiola yupo Manchester City, Jose Mourinho anainoa Manchester United na Antonio Conte ametulizana na Chelsea.
Mashabiki wanapata burudani ya kutosha kutoka kwa makocha kupitia kwa wachezaji wa vikosi vya kwanza kwenye timu zao. Kila kocha anajaribu kuonyesha makali yake. Kwenye hilo la ushindani wa makocha, linaleta ushindani kwa wachezaji na kufanya kuwapo na mastraika matata wanaolazimika kuanzia kwenye benchi.
Hata hivyo, kuanzia benchi haijawahi kuwa shinda kwa baadhi ya washambuliaji kutokana na kufunga mara nyingi baada ya kuanzia kwenye benchi.
6.Olivier Giroud- mabao 13
Straika wa Chelsea, Olivier Giroud amefunga mabao 73 katika mechi 185 alizocheza Ligi Kuu England. Fowadi huyo Mfaransa alikuwa na madhara makubwa chini ya Kocha Arsene Wenger kutokana na uwezo wake wa kuusoma mchezo akiwa benchi kisha anapoingia tu, anakwenda kufanya mabadiliko. Giroud aliwekwa benchi mara nyingi sana, lakini mara zote alizoingia alionyesha uwepo wake ndani ya uwanja na amefunga mara 13 katika mechi 52 alizoingia kutokea kwenye benchi. Kocha Antonio Conte akitaka kumfaidi zaidi staa huyo basi aendelee kumchezesha kama super sub.
5.Javier Hernandez- mabao 14
Fowadi wa zamani wa Manchester United, Javier Hernandez anafahamika kama super sub. Kocha Sir Alex Ferguson alimtumia kwenye hilo mara nyingi sana. Alitua kwenye klabu hiyo alitokea Mexico alikuwa akianzishwa, lakini baadaye kocha huyo wa Man United aligundua Hernandez maarufu kama Chicharito ni mzuri zaidi akiwa anatokea benchi. Ferguson alifanya uamuzi sahihi kwa sababu staa huyo alifunga mabao 14 katika mechi 54. Hiyo pia inahusisha katika kipindi chake alichokuwa chini ya Kocha David Moyes na kidogo sana chini ya Louis Van Gaal. Kwa sasa yupo West Ham alikojiunga akitokea Bayer Leverkusen.
4.Daniel Sturridge- mabao 15
Straika wa West Brom, Daniel Sturridge anayecheza huko kwa mkopo akitokea Liverpool ni mmoja wa wachezaji ambao wamefunga mara nyingi wakiwa wanatokea benchi.
Majeraha yamekuwa yakimsumbua sana na pengine hilo linaweza kuwa sababu ya kuwafanya makocha wake wawe wanamwanzia benchi ili asiumie zaidi. Lakini, jambo hilo halikumfanya Sturridge kushindwa kuonyesha uwezo wake wa kutupia wavuni baada ya kufunga mabao 15 katika mechi 78 alizocheza akitokea benchi. Bado kuna kitu cha kuvuna kutoka kwake na huenda akapata timu mpya mwishoni mwa msimu.
3.Nwankwo Kanu- mabao 17
Staa wa Arsenal, Nwankwo Kanu naye alikuwa super sub kwenye kikosi hicho cha Arsene Wenger. Alifunga mabao 17 katika mechi 118 ambazo alianzia benchi katika kikosi hicho cha Arsenal. Alidumu kwa misimu sita yenye mafanikio makubwa huko Arsenal, akishinda mataji mawili ya Ligi Kuu na mawili ya Kombe la FA.
Alikuwamo kwenye kikosi kikosi cha Arsenal kisichofungika mwaka 2004. Kanu ni mmoja kati ya wanasoka wachache wa Kiafrika ambao walibeba taji la Ligi ya Mabingwa Ulaya baada ya kufanya hivyo akiwa na Ajax iliyokuwa chini ya Kocha Louis Van Gaal.
Mabao yake ya kuanzia benchi yanahusisha pia kipindi chake alichokuwa West Brom na Portsmouth.
2.Ole Gunnar Solskjaer- mabao 17
Gwiji wa Manchester United, Ole Gunnar Solskjaer atakumbukwa sana kwa kile alichokifanya kwenye fainali ya Ligi ya Mabingwa Ulaya mwaka 1999.
Ndiye mchezaji aliyewaduwaza Bayern Munich na kuipa timu yake ya Man United ubingwa wa taji hilo. Mashabiki wa Man United wanapaswa kufahamu staa wao huyo alikuwa super sub.
Alifunga mabao 17 katika mechi 84 alizoanzia kwenye benchi. Kwa jumla, Solskjaer alifunga mabao 126 katika mechi 366 alizoichezea Man United kwa misimu 11.
1.Jermain Defoe- mabao 23
Straika wa Bournemouth, Jermain Defoe hakuna ubishi ni gwiji Ligi Kuu England. Amefunga mabao 272 katika mechi 669 alizochezea kwenye vikosi vya Tottenham Hotspur, West Ham, Portsmouth na Sunderland. Ni mmoja wa washambuliaji bora kabisa kwenye ligi kwa muongo huu.
Defoe anashikilia rekodi ya kuwa mchezaji aliyefunga mabao mengi akitokea benchi baada ya kufunga mara 23 katika mechi 103 alizoanzia nje ya kikosi cha kwanza.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here