Wachezaji Stars jiongezeni- Mkwasa

0
10

KOCHA wa zamani wa timu ya soka ya Taifa, Taifa Stars, Charles Mkwasa amewataka wachezaji wa timu hiyo kujiongeza wawapo uwanjani badala ya kumtegemea kocha wao kwa kila kitu.

Mkwasa ambaye kwa sasa ni katibu mkuu wa Yanga ameyasema hayo baada ya Stars kufungwa mabao 4-1 na Algeria mjini Algiers katika mechi ya kimataifa ya kirafiki juzi.

Mkwasa aliwahi kuwa kocha wa timu hiyo ilipofungwa mabao 7-0 na Algeria katika mechi ya kufuzu kombe la dunia.

Akitoa tathmini ya mchezo huo juzi, wachezaji wa timu hiyo walionekana kuzidiwa sehemu kubwa na kucheza chini ya kiwango dhidi ya wapinzani wao.

“Kuna mambo mengine mchezaji anatakiwa kujiongeza mwenyewe unapoona mambo yamebadilika kwenye mechi, siyo lazima ufanye vilevile alivyofundisha mwalimu, unatakiwa kutumia uwezo wako binafsi wakati mwingine,” alisema Mkwasa.

Aidha, kuhusu kuchagua wachezaji wa timu ya taifa, Mkwasa alisema kila mwalimu anakuwa na mipango yake lakini katika kuchagua wachezaji kama hawana uzoefu na michezo mikubwa basi inaweza kujirudia historia iliyompata akiwa kama kocha wa Taifa Stars.

“Mchezaji kama Samatta (Mbwana) na wengine, wangepewa fursa ya kupumzika ili wengine wacheze wapate uzoefu maana hata Algeria wachezaji wao waliotufunga goli saba ni wachache sana waliocheza,” alisema Mkwasa.

Alisema ni bora kuwa na wachezaji wengi ambao wanacheza ligi mbalimbali ili waweze kuisaidia timu yao wanapohitajika kwenye majukumu ya timu ya Taifa, kwani hata Algeria imesheheni wachezaji wengi kutoka nje ya Ligi yao.

Taifa Stars imesheheni wachezaji wengi wa ligi ya ndani, kitu ambacho katibu huyo alisema hakiwezi kuisaidia timu hiyo katika mashindano tofauti.

“Ukiangalia Algeria angalia vilabu vyao vinafika wapi kwenye mashindano ya Afrika ni mbali sana kwa hiyo kuna haja pia ya kuwatengeneza wachezaji wetu kuwa na ubora zaidi,” aliongeza Mkwasa.

Chanzo: Habarileo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here