Twiga Stars yalilia kujipima kimataifa

0
2

WAKATI kikosi cha timu ya soka ya Taifa ya Wanawake (Twiga Stars) kikiwa kinajiandaa na mashindano ya Kombe la Chalenji, Kocha Msaidizi wa timu hiyo, Edna Lema, amesema wanahitaji kupata mechi za kujipima nguvu za kimataifa kabla ya kuelekea kwenye michuano hiyo.
Twiga Stars itasafiri kwenda Kigali, Rwanda kutetea ubingwa wa Kombe la Chalenji kwa nchi za Afrika Mashariki na Kati katika mashindano yatakayofanyika mapema Mei mwaka huu.

Lema aliliambia gazeti hili kuwa wachezaji wake wanaendelea vyema na mazoezi, lakini wakipata mechi za kimataifa itawasaidia kufahamu makosa yaliyopo na vile vile zitawajenga kiufundi.

“Hatujapata mechi za kirafiki tangu tulipocheza na Cameroon mwaka juzi, kucheza na timu za wanaume au klabu si kipimo sahihi kwetu, sasa hivi soka la wanawake limekuwa na kila mmoja anataka kuona anaifunga Tanzania, awali walitudharau, lakini sasa wamejipanga,” alisema Lema.

Kiungo huyo wa zamani wa Twiga Stars, alisema kuwa licha ya changamoto zilizopo, anawapongeza wachezaji wake kwa kufuata na kutekeleza programu za mazoezi zilizopangwa na benchi la ufundi la timu hiyo iliyoko chini ya Sebastian Nkoma.

Twiga Stars ndio mabingwa wa kwanza wa mashindano ya Kombe la Chalenji yaliyofanyika mwaka juzi Jinja, Uganda chini ya usimamizi wa Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati (CECAFA).

Source:IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here