Timu ya taifa yatwaa mil 22 Hispania

0
6

TIMU ya taifa ya riadha ya Uganda imetwaa kiasi cha dola za Marekani 6,000 (sawa na Sh milioni 22 za Uganda) baada ya kushika nafasi ya tano katika mashindano ya dunia ya nusu marathon mwishoni mwa wiki Valencia, Hispania.

Kwa miaka mingi, Uganda imekuwa ikisubiri medali kwa mchezaji mmoja mmoja katika mashindano hayo ya dunia ya nusu marathon, ambapo sasa itabidi kuendelea kusubiri medali hiyo hadi mwaka 2020 Gdynia, Poland.

Kwa mara nyingine, taifa hilo la Afrika Mashariki limeshindwa kupata nafasi ya kupanda stejini kutokana na kuendeleza ukame wa medali katika mashindano haya ya riadha, ambapo kwa mara ya mwisho ilipata medali mwaka 2004 wakati wanariadha watatu, Wilson Busienei, Martin Toroitich na Joseph Nsubuga waliposhinda medali ya shaba kwa timu mjini New Delhi, India.

Jumamosi, Uganda ilitwaa kiasi hicho cha fedha baada ya kushika nafasi ya tano kwa upande wa timu katika mbio za wanaume za kilometa 21, mbio ambazo mshindi ni Mkenya, Geoffrey Kamworor aliyeshinda mbio hizo kwa mara ya tatu mfululizo.

Kamworor, ambaye alichomoka kwa kasi zikiwa zimebaki kilometa nne kabla ya kumalizika kwa mbio hizo, alishinda kwa kutumia saa 1:02 na kuongeza taji la mwaka 2014 na 2016 huko Copenhagen na Cardiff.

Hatahivyo, bado Fred Musobo ndiye mwanariadha bora wa Uganda baada ya kumaliza katika nafasi ya 20 baada ya kuposti muda wake bora binafsi wa saa 1:01:38. Hilo lilimfanya kocha wa Uganda, Gordon Ahimbisibwe kutamka awali kuwa Kenya walikuwa wakiihofia Uganda kabla ya kufanyika kwa mbio hizo.

Chakuvutia zaidi, Jackson Kiprop ndiye mwanariadha wa mwisho wa Uganda kumaliza ndani ya 10 bora wakati alipomaliza katika nafasi ya saba katika mashindano yaliyofanyika Karvana, Bulgaria miaka sita iliyopita.

Ethiopia iliiongoza Kenya na Bahrain katika orodha ya medali katika timu kwa upande wa wanaume na wanawake, ambapo Jemal Yimer, Getanneh Molla na Betesfa Getahun walikosa nafasi ya kupanda stejini lakini walimaliza katika nafasi ya nne, tano na sita.

Kwa upande wa wanawake, Muethiopia Netsanet Kebede kidogo avunje rekodi ya dunia kwa sekunde 14 alipomaliza kwa kutumia saa 1:06:11, wakishinda zawadi ya dola za Marekani 50,000.

Source:Habarileo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here