Simba Yaitafutia Kasi Mpya Njombe

0
3

KIKOSI cha Simba kinatarajia kuanza mazoezi Jumamosi kwa ajili ya kuikabili Njombe Mji katika mechi ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayopigwa Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Saba Saba mkoani Njombe.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, imerejea kwenye Ligi Kuu baada ya Jumamosi iliyopita kutolewa na Al Masry ya Misri katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Simba, Haji Manara, alisema kuwa kabla ya mechi hiyo, huenda kikosi chao kikacheza mechi moja ya kirafiki yenye lengo la kuwaweka wachezaji tayari na vita ya kusaka pointi tatu.
Manara alisema kuwa wanataka kuona kikosi chao kinaendeleza kucheza kwa kiwango bora kama walichokionyesha kwenye mechi zote mbili za kimataifa hivi karibuni.
“Wachezaji walikuwa na mapumziko mafupi baada ya kurejea nchini, wataanza mazoezi tena Jumamosi, na kama mambo yatakwenda vyema tunaweza kuwa na mchezo mmoja wa kirafiki kabla ya kuelekea Njombe, tunataka wachezaji wawe na “fitness” ya juu na kuendeleza mapambano,” alisema Manara.
Aliongeza kuwa wanafuraha kuona wachezaji wao waliokuwa majeruhi wakiwa wamepona na kuungana na wenzao kwenye mazoezi kwa ajili ya kupambana katika mechi zilizosalia za ligi.
Baada ya mechi dhidi ya Njombe Mji, Simba itaelekea Morogoro kuwafuata wenyeji wao Mtibwa Sugar katika mchezo mwingine wa Ligi Kuu Bara utakaofanyika Aprili 8, mwaka huu kwenye Uwanja wa Jamhuri.
Wekundu wa Msimbazi ambao wana mechi mkononi ndio timu pekee haijapoteza mchezo hata mmoja huku wakiwa wanaongoza katika msimamo wa ligi wakifuatiwa na mabingwa watetezi Yanga ambao pia wana pointi 46 na Azam FC wenye pointi 40 wako katika nafasi ya tatu.

Na Vicent Segona vicent@spoti.co.tz
Source: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here