Simba yaishika Yanga pabaya

0
3
Hesabu za kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Tanzania Bara, zimekuwa kali hasa baada ya Yanga kuangukia kwenye Kombe la Shirikisho Afrika baada ya Simba kuondolewa.
Yanga imeingia kwenye hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho ambapo itacheza na Welayta Dicha ya Ethiopia, baada ya kutolewa kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika na Township Rollers ya Botswana.
Mabingwa hao wa Ligi Kuu wakifuzu wataingia kwenye hatua ya makundi ya mashindano hayo ambayo Simba ilishiriki kabla ya kuondolewa na Al Masry ya Misri kwenye hatua ya raundi ya kwanza.
Kitendo cha Yanga kushiriki Kombe la Shirikisho Afrika, kutoa fursa kwa timu hiyo kuwania mataji matatu yakiwemo Kombe la FA na Ligi Kuu Tanzania Bara.
Yanga inaipumulia Simba baada ya kufikisha pointi 46 sawa na timu hiyo, lakini ina uwiano mzuri wa idadi ya mabao ya kufunga na kufungwa.
Ushiriki wa Yanga kwenye mashindano matatu unaweza kuiathiri kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu kwasababu baadhi ya nyota muhimu wanaweza kupata majeraha au kuchoka jambo linaloweza kuifaidisha Simba.
Yanga ina kikosi ambacho sio kipana, hivyo endapo wachezaji watapata majeraha au kuchoka inaweza kujikuta kwenye wakati mgumu kulinganisha na wapinzani wao ambao wanajivunia kundi kubwa la wachezaji wenye uwezo mzuri.
Lakini faida inayoweza kuwabeba Yanga katika Ligi Kuu kutokana na ushiriki wake kwenye mashindano matatu makubwa tofauti, ni kuongeza ufiti kwa wachezaji wake.
Kwa upande wa Simba, kitendo cha kutupwa nje kwenye Kombe la Shirikisho kinaongeza presha kwa kuwa tegemeo lao ni ubingwa wa Ligi Kuu pekee ili kushiriki mashindano ya kimataifa mwakani.
Hata hivyo, kwa upande mwingine Simba inaweza kunufaika kutolewa Kombe la Shirikisho kwa sababu nguvu kubwa itazihamishia kwenye Ligi Kuu na itakuwa na wigo mpana wa kuibana Yanga.
Kocha msaidizi wa Simba, Masoud Djuma alisema lengo la kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu liko palepale licha ya kukabiliana na changamoto.
“Kuna ugumu wa kutwaa ubingwa wa Ligi. Tutaendelea kufanya kazi kwa pamoja na kushirikiana ili kuhakikisha tunafanikiwa,” alisema Djuma.
Kocha wa Yanga, George Lwandamina alidai mkakati wao ni kufanya vizuri na kutwaa ubingwa wa mashindano yote.
“Tulikuwa tunasubiri kuona tutapangwa na timu gani kwenye Kombe la shirikisho Afrika, imeshafahamika,” alisema Lwandamina.
Wasikie wadau
“Simba wapo kwenye nafasi ya kuchukua ubingwa kama watatulia, lakini endapo wakivurugana wataishia kuusikia. Yanga imekuwa na hesabu nzuri za namna ya kumaliza msimu,” alisema Ulimboka Mwakingwe, nyota wa zamani wa Simba.
Nyota wa zamani wa Yanga, Sekilojo Chambua alisema timu hiyo haiwezi kuathiriwa na ushiriki wao kwenye mashindano mengine ikiwemo Kombe la Shirikisho Afrika.

Chanzo: Mwananchi

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here