Saturday, August 18, 2018
Home Sports Simba waanika mbinu za ubingwa

Simba waanika mbinu za ubingwa

0
3
KOCHA Msaidizi wa Simba, Masoud Djuma, amesema watautumia vyema muda ambao timu hiyo haina mechi za kimataifa na Kombe la FA kurekebisha makosa ya kiufundi waliyoyabaini ili warejee kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara wakiwa na kasi.
Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo ya Michezoni ya SportPesa, itaanza mazoezi kesho kwa ajili ya kujiandaa na mechi yao dhidi ya Njombe Mji FC itakayopigwa Aprili 3, mwaka huu kwenye Uwanja wa Saba Saba mkoani Njombe.
Akizungumza na gazeti hili jana, Djuma, alisema wanataka kuona hawapotezi pointi katika mechi zao tisa zilizobakia na hatimaye wanafanikiwa kutwaa ubingwa wa ligi msimu huu.
Djuma alisema wanataka kukiimarisha zaidi kikosi chao kwa sababu hatua iliyobaki ni ngumu zaidi kutokana na vita ya kuwania ubingwa na ile ya kushuka daraja kufanana.
“Tunaelekea mwisho wa ligi, huku ni kugumu zaidi na ndio tunahitaji kushinda, ukipoteza pointi, basi umempa nafasi mpinzani wako, hatutaki kuona tunapoteza hii nafasi iliyobaki ya kushinda taji msimu huu,” alisema kocha huyo raia wa Burundi.
Aliongeza kuwa mechi zote zilizobaki kwenye ligi ni ngumu na wanawakumbusha wachezaji wao kutobweteka au kuingia uwanjani na matokeo ya mzunguko wa kwanza.
Kikosi hicho kinachoongozwa na Mfaransa, Pierre Lenchatre, kimerejea kwenye Ligi Kuu kamili baada ya kuondolewa katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika na Al Masry ya Misri ambayo ililazimisha sare ya mabao 2-2 walipokutana Machi 7, mwaka huu jijini Dar es Salaam na kutoka suluhu ugenini.
Simba ndio wanaongoza katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 16 wakifuatiwa na mabingwa watetezi, Yanga ambao pia wana pointi 46, lakini wakizidiwa kwa tofauti ya mabao ya kufunga na kufungwa, huku Azam FC wenye pointi 40 wakiwa katika nafasi ya tatu.


Na vIcent Segona vicent@spoti.co.tz

Chanzo: IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here

}