Samatta Awatuliza Mashabiki

0
4

NAHODHA wa timu ya taifa ya Tanzania, Mbwana Samatta amewataka mashabiki wa timu hiyo kutochoka kuishangilia timu hiyo licha ya kipigo cha mabao 4-1, dhidi ya Algeria.

Juzi Stars ilipoteza kwa mara ya pili mfululizo dhidi ya miamba hiyo ya Afrika ukiwa ni mchezo wa kirafiki wa Kimataifa uliopo kwenye kalenda ya FIFA, Shirikisho la Kimataifa la Soka.

Akizungumza kwa njia ya mtandao kutoka Algeria, ambako mechi hiyo ilipochezwa, Samatta alikiri kuwa matokeo hayo ni mabaya kwao lakini akasema watajitahidi kupambana ili kufanya vizuri kwenye mechi zijazo ikiwemo ile ya DR Congo watakayocheza Jumanne ijayo Uwanja wa Taifa Dar es Salaam.

“Ni kweli matokeo siyo mazuri kwetu ingawa lengo letu lilikuwa ushindi lakini Watanzania hawapaswi kukata tamaa kwa sababu tumecheza na timu kubwa Afrika kitu cha msingi waendelee kutusapoti kwani tunaimarisha timu kwa ajili ya kufanya vizuri kwenye michuano ya kufuzu fainali ya Mataifa ya Afrika,” alisema Samatta.

Nahodha huyo ambaye anakipiga kwenye klabu ya KRC Genk inayoshiriki Ligi Kuu nchini Ubelgiji alisema pamoja na kupoteza mchezo huo, lakini timu yao ilijitahidi kucheza vizuri na wana matumaini ya kufanya vizuri kwenye mchezo wao mwingine wa kirafiki na Congo.

Samatta mbali na kukiri kukutana na timu bora Afrika lakini pia kikosi chao kilitumia baadhi ya wachezaji wapya ambao ndiyo ilikuwa mara yao ya kwanza kuichezea timu hiyo.

Kikosi cha Stars kinatarajiwa kuwasili nchini leo tayari kwa ajili ya pambano lake la Jumanne dhidi ya Congo ukiwa ni mchezo wao mwisho wa kirafiki kwa mwezi huu katika kalenda ya FIFA

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here