Okwi atengewa bilioni 1.2

0
8
ACHANA na matokeo ya usiku wa jana ya Simba na Al Masry katika mechi ya marudiano ya Kombe la Shirikisho Afrika, Waarabu hao wa mji wa Port Said, wamevutiwa na kiwango cha straika Emmanuel Okwi.
Tayari Waarabu wameanza harakati za chini kwa chini ili kuuvunja mkataba wa Mganda huyo kwa Wekundu wa Msimbazi hao.
Viongozi wao wamewasiliana na baadhi ya vigogo wa Simba kutaka kujua kipengele cha mauzo ya Okwi kwenye mkataba wake ni kiasi gani ili waweze kufanya mambo.
Waarabu hao tayari wamefahamishwa kuwa kuvunja mkataba wa Okwi na Simba ni Dola 600,000 (Sh1.2 bilioni) na sasa imebaki kazi kwao kuamua mbichi ama mbivu.
Mmoja wa watu wa Al Masry, alisema huenda klabu hiyo ikafanya kweli ama kuzungumza na Simba ili kushusha bei hiyo kwa kuwa hawataki kumkosa staa huyo anayeichezewa pia timu ya taifa ya Uganda, The Cranes.
Kaimu Rais wa Simba, Salim Abdallah ‘Try Again’ amesema hawana tatizo kumuuza staa huyo kwani tayari pia wana ofa nyingine mezani tena ya dau nono zaidi.
“Al Masry bado hawajaleta ofa yoyote, ila kama wanamtaka Okwi waje tu mezani, hatuwezi kukataa fedha kama ni nzuri,” alisema Try Again.
“Kuna timu imekuja pia ikauliza tunaweza kuwapa Okwi kwa kiasi gani, nimewaambia Dola 1.2 milioni (Sh2.6 bilioni) hivyo wamekwenda kujipanga pia, ni timu ya nje.
“Ni kweli Okwi amekuwa msaada mkubwa kwetu, lakini kama ofa itakuwa nzuri tutamuuza. Tunajua kwamba tunaweza kupata wachezaji wengine wazuri pia, wakaziba nafasi yake.”
Endapo dili hilo la Okwi litafanikiwa, Simba itakuwa inamuuza staa huyo kwa mara ya tatu kwani, awali ilimuuza kwenda Etoile Du Sahel ya Tunisia na baadaye Sondersjke ya Denmark.
Katika mauzo ya awali, Simba ilimuuza Okwi kwa dola 300,000 (Sh680 milioni kwa sasa) kwenda Etoile mwaka 2013. Hata hivyo, fedha hizo zililipwa miaka minne baadaye.
Simba ilimuuza tena Okwi kwa dola 200,000 (Sh440,000 kwa sasa) kwenda Sondersjke ya Denmark mwaka 2015.
Kwa sasa huenda Okwi akaweka rekodi mpya ya mauzo tofauti na awali kutokana na kiwango chake kuimarika maradufu.
Okwi ameifungia Simba mabao 19 katika mashindano yote hadi sasa msimu huu hivyo kuwa nyota mwenye mchango zaidi klabuni hapo.
Kapombe freshi
Katika hatua nyingine kiraka wa Simba, Shomari Kapombe, amesema hana tatizo na nafasi ya kiungo ambayo kocha Mfaransa, Pierre Lechantre amekuwa akimtumia kwa sasa.
Kapombe, ambaye kwa kawaida huwa anacheza beki ya kulia, ameanza kuchezeshwa kiungo mshambuliaji, nafasi ambayo hakuwahi kuicheza hapo kabla.
Nyota huyo wa zamani wa Azam na AS Cannes ya Ufaransa, alisema amekuwa akifuata maelekezo ya kocha na kucheza popote anapopangwa bila kujali nafasi ipi ameizoea zaidi.
“Kikubwa ni kwamba nafanya kile ambacho mwalimu amenielekeza, kucheza kiungo wala siyo tatizo kwangu,” alisema Kapombe.
Kwa upande mwingine, alisema anafurahi kuitwa tena kwenye kikosi cha Taifa Stars ikiwa ni wiki chache tu baada ya kutoka benchi la majeruhi.
Nyota huyo alikosekana kwenye kikosi cha Stars tangu alipoumia Julai mwaka jana, lakini amejumuishwa kwa mara nyingine tena kwenye timu itakayocheza mechi mbili za kirafiki dhidi ya Algeria na DR Congo.
“Namshukuru Mungu nimeweza kurejea na kiwango changu kupanda kwa haraka hadi kuitwa tena timu ya Taifa, ni jambo la faraja kwangu, cha muhimu kwangu ni kujituma zaidi.” alisema.
Source: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here