Misri yauvaa muziki wa Ureno

0
2

Cairo, Misri. Mwanasoka bora wa Afrika, Mohamed Salah ataonyeshana kazi na mwanasoka bora wa Dunia, Cristiano Ronaldo katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa utaozikutanisha Misri na Ureno leo Ijumaa kwenye Uwanja wa Letzigrund, Uswisi.
Timu hizo zinautumia mchezo huo katika maandalizi yao ya kuelekea katika Kombe la Dunia 2018 litakalofanyika Russia kati ya Juni na Julai.
Utamu wa mchezo huo unaongezwa na uwepo wa Mo Salah wa Misri na Ronaldo ambao kwa sasa wanatikisa dunia kwa kasi yao ya upachikaji mabao.
Salah anakwenda katika mchezo huo akiwa amefunga mabao 36 katika mechi 40 alizocheza na  ya mashindano yote hadi sasa kwa timu ya taifa na klabu yake ya Liverpool.
Ronaldo amekuwa moto wa kuotea mbali tangu kuanza kwa mwaka huu tayari amefunga mabao 21 katika mechi 13 za mashindano yote alizocheza.
Timu hizo zimekutana mara tatu Ureno imeshinda mechi mbili na Misri ikishinda mechi moja hivyo wanaingia uwanjani wakitaka kuweka rekodi hiyo sawa.
Misri kwa sasa ipo nafasi ya 44 kwenye viwango vya ubora wa Fifa wakati Ureno mabingwa wa Ulaya wakiwa nafasi ya tatu katika viwango hivyo.
Misri mechi yake ya mwisho ya kimataifa iliyochezwa Novemba mwaka jana ililazimishwa sare 1-1 na Ghana iliyopa tiketi ya kucheza Kombe la Dunia.
Mabingwa hao mara saba wa Afrika, Misri hawajafunga katika michezo mitatu iliyopita ya mashindano yote.
Mafarao wanaofundishwa na kocha Muargentina, Hector Cuper wanarekodi ya kushinda mechi mbili na kutoka sare moja ya hivi karibuni.
Wapinzania wao Ureno wenyewe walitoka sare 1-1 na Marekani katika mechi yake ya kirafiki iliyochezwa Novemba mwaka jana.
Sare hiyo imewafanya mabingwa hao wa Ulaya kuweka rekodi ya kutokufungwa katika michezo saba iliyopita ya mashindano yote.
Ureno ‘Selecton’ inayofundishwa na kocha Mreno Fernando Santos, wamefanikiwa kushinda mechi sita na kupata sare mmoja katika michezo yake ya karibuni.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here