Mayanga: Timu ngumu zinaiboresha Taifa Stars

0
5
KOCHA Mkuu wa timu ya soka ya Tanzania (Taifa Stars), Salum Mayanga, amesema kuwa kucheza mechi na mataifa yaliyoendelea kunasaidia kuiboresha timu yake na anaamini itafika wakati matunda mazuri yataonekana.
Taifa Stars imetoka kupoteza mechi ya kirafiki dhidi ya Algeria na kesho inatarajia kuikaribisha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) katika mechi nyingine ya kirafiki itakayopigwa kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam.
Akizungumza na gazeti hili jana, Mayanga, alisema kuwa Stars inapocheza na “timu ngumu” ndio inapata nafasi ya kujiimarisha na kujijenga tofauti na awali ilipokuwa inacheza na mataifa ambayo wamepishana kiwango kidogo cha ubora.
Mayanga alisema pia anaamini mechi ya kesho dhidi ya DRC itawapa nafasi nyota wake kuendelea kujifunza kutokana na kikosi hicho kuundwa na wachezaji wanaocheza ligi mbalimbali hapa duniani.
“Kiukweli mechi hizi dhidi ya timu zilizoendelea ni nzuri na zinatujenga, wachezaji wanajifunza mengi na naamini makosa waliyokuwa wanayafanya yatapungua kupitia wanavyoona wenzao wanavyocheza, nimefurahi kupata nafasi ya kujipima na Algeria na Jumanne tutakapoikaribisha Kongo,” alisema Mayanga.
Aliongeza kuwa bado wachezaji wa Tanzania wanakosa uzoefu kutokana na kukosa mechi nyingi za mashindano huku wakiwa kwenye klabu wanapambana na changamoto za ndani na nje ya uwanja.

Chanzo: IPPmedia

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here