Lechantre amuwahi Benitez Dar

0
7
KOCHA wa Simba, Mfaransa Pierre Lechantre, aliamua kupitiliza juu kwa juu kwao ili kupumzika mara baada ya chama lake kutolewa na Al Masry ya Misri katika michuano ya Kombe la Shirikisho barani Afrika, lakini ghafla tu kajikuta amekatwa stimu.
Hii ni baada ya kujulishwa kuwa, Kocha Ali Bushir ‘Benitez’ anayeinoa Njombe Mji anamsubiri kwa hamu katika pambano lao la Ligi Kuu Bara litakalochezwa Aprili 3 mjini Njombe, hivyo kuamua kumwahi mapema ili kila kiti kiwe sawa ugenini.
Simba isiyo na michuano mingine yoyote inayoshiriki sasa zaidi ya Ligi Kuu, imepangwa kukutana na Njombe katika mechi ya kiporo, jambo ambalo limemfanya Lechantre kuharakisha kuwahi Dar es Salaam ili kuwapa dozi nene vijana wake.
Kocha huyo anatarajiwa kutua nchini leo Jumapili na moja kwa moja ataanza kazi ya kukinoa kikosi chake ambacho kilishaanza kujifua tangu jana jioni kuelekea katika mechi dhidi ya vijana wa Benitez ambao walifumuliwa mabao 4-0 jijini Dar.
Lechantre alipewa mapumziko ya wiki moja na mabosi wake mara baada ya mchezo wao na Al Masry uliopigwa ugenini mjini Port Said na kumalizika kwa suluhu baada ya sare ya 2-2 nyumbani wiki moja kabla na Wekundu kutolewa.
Meneja wa Simba, Richard Robert ‘Mwana’ alisema Lechantre anatarajia kuingia asubuhi ya leo Jumapili na moja kwa moja atakwenda kupumzika na jioni ataungana na timu inayojifua kwenye Uwanja wa Boko Veterans.
Robert alisema walianza mazoezi jana chini ya Kocha Msaidizi Masudi Djuma, akisaidiana na kocha wa viungo Mohammed Habib wakiwa na nyota wachache kwani, wengi wao wapo kwenye majukumu yao timu za taifa.
“Kurudi kwa kocha tuna imani ataongeza kitu kwani, alikuwa mapumzikoni baada ya mechi ngumu na Al Masry na hata wachezaji nao walikuwa na mapumziko ya kutosha, lakini tumerudi kazini kwa maandalizi makali.
BENITEZ NOMA
Naye Benitez tangu atue Njombe ameifanya timu hiyo kuwa tishio akiivusha robo fainali ya Kombe la FA, pia ikiwa imepoteza mechi moja tu kati ya tano alizoiongoza.
Mechi hizo zinajumuisha nne za Ligi Kuu na moja ya Kombe la FA na wikiendi hii itashuka uwanjani kuvaana na Stand United kusaka nafasi ya kutinga nusu fainali ya FA.
Benitez, ambaye alikuwa kipa tegemeo wa Taifa Stars, pia amewahi kuzinoa Mwadui na Polisi Tanzania na kuzifanya timu hizo kuwa imara kwa kile kinachoelezwa ni misimamo yake mikali ya kutopenda kuingiliwa kazini.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here