Kocha Stars atetea kichapo

0
10

KOCHA wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ Salum Mayanga amesema mechi dhidi ya Algeria licha ya kupoteza wamejifunza vitu muhimu na kuahidi kuvifanyia kazi ili kutorudia makosa yao.

Katika mchezo huo wa kimataifa wa kirafiki uliochezwa juzi kwenye uwanja wa 5 Julliete 1962 huko Algeria, Stars ilikula kichapo cha mabao 4-1.

Akizungumza na gazeti hili kwa njia ya simu, Mayanga amesema, mchezo ulikuwa mzuri, japo una matokeo ya kufungwa lakini vitu vya kiufundi na kimbinu vitawasaidia kuboresha mchezo unaofuata dhidi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).

“Mchezo ulikuwa mzuri kwa sababu tumejifunza, kikubwa tulicheza na timu yenye kiwango cha juu hasa kwenye maamuzi walikuwa wepesi sana na makosa tuliyoyafanya waliyatumia kwa haraka sana na kuweza kupata ushindi,” amesema.

Amesema matokeo hayawezi kuwakatisha tamaa kwani ni muda mrefu walitafuta timu kubwa kwa ajili ya kucheza nayo na kwamba jukumu lake ni kuona mechi kubwa zinawaimarisha.

Timu hiyo inatarajiwa kutua leo ikitokea Algeria kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wa pili wa kimataifa wa kirafiki utakaochezwa Jumanne ijayo kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Mayanga amesema watakaporejea, atahakikisha anafanya masahahisho ya makosa yaliyojitokeza katika mchezo huo uliopita.
Amesema anakiamini kikosi chake bado kina uwezo wa kucheza kwa kiwango bora dhidi ya DR Congo.

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here