Klabu ya Simba yarejea mawindoni

0
5

TIMU ya Simba iliyokuwa mapumzikoni kwa takriban siku tano, jana ilitarajia kuanza rasmi maandalizi yake kwa ajili ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu Bara msimu huu, michuano pekee ambayo wamesalia katika msimu huu.

Kikosi cha Simba kilipewa mapumziko tangu kiliporejea kikitokea Misri kuumana na Al Masry kwenye michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika ambapo walipata suluhu lakini walitupwa nje ya mashindano hayo kutokana na matokeo ya mechi ya awali ya sare ya 2-2 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar.

Meneja wa Wekundu hao, Richard Robert amesema, wameamua kurejea mapema kuanza maandalizi hayo kwa kutambua uhitaji wao wa ubingwa wa Ligi Kuu msimu huu ambapo wamedhamiria kuondoka na pointi zote 30 za mechi 10 walizobakisha kabla ya kumalizika kwa ligi hiyo.

“Unajua tunahitaji kufanya maandalizi haya mapema maana kama unavyoona tumesaliwa na ushiriki katika ligi tu kwa hiyo lazima tuweke nguvu zetu zote hapa na kupambana vya kutosha kuhakikisha tunaondoka na pointi zote 30 zilizobaki ili kutwaa ubingwa bila wasiwasi,” amesema Robert.

Pamoja na hayo, Robert alieleza kuwa watafanya mazoezi hayo kwa siku mbili kabla ya kesho kuanza rasmi kambi ya kujiwinda dhidi ya timu ya Njombe Mji wanayotarajia kucheza nayo April 3, mwaka huu katika Dimba la Sabasaba mkoani Njombe.

Meneja huyo pia aligusia kuhusu kurejea kwa kocha wao Mfaransa, Pierre Lechantre ambaye anatarajia kutua nchini leo akitokea Ufaransa alikokwenda kwa ajili ya mapumziko mafupi mapema baada ya kumalizika kwa mechi yao dhidi ya Masry.

“Timu itaingia kambini Jumatatu (kesho) na hata wachezaji ambao wapo timu za taifa, wataungana na timu mapema baada ya kumaliza majukumu yao katika timu zao za taifa ili kukamilisha lengo letu kwa ufanisi mkubwa.

“Hata kocha Lechantre tunatarajia atatua nchini kesho (leo) kwa ajili ya kuiwahi timu na kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa na hakuna kinachoharibika kulingana na matarajio tuliyonayo,” alisema.

Mpaka sasa Simba yenye maskani yake Mtaa wa Msimbazi na Kariakoo Dar es Salaam inaongoza ligi kwa uwiano mzuri wa mabao ikiwa na pointi 46 sawa na mabingwa watetezi, Yanga wanaoshika nafasi ya pili.

Simba imebakiwa kwenye mbio za ubingwa wa Ligi Kuu pekee baada ya kutupwa nje kwenye michuano ya kombe la Shirikisho la Azam katika raundi za mapema.

Chanzo: Habarileo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here