Hiki ndicho kimetokea Taifa Stars ikilala mabao 4-1

0
3
Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ imekubali kipigo cha mabao 4-1 katika mchezo wa kirafiki wa kimataifa uliocheza jana Alhamisi usiku nchini Algeria.
Bao la kwanza la Algeria lilifungwa katika dakika ya 13 na mshambuliaji Baghdad Bounedjah akimalizia vizuri pasi kutoka kwa Riyad Mahrez.
Tanzania ilifanikiwa kusawazisha bao hilo kupitia kwa Saimon Msuva katika dakika ya 21 akipokea pasi kutoka kwa Said Ndemla na kufanya matokeo kuwa 1-1.
Kikosi cha Stars kilijikuta katika giza baada ya beki Shomari Kapombe dakika ya 44 kujifunga wakati akijaribu kuokoa mpira kwa kichwa kufanya timu hizo kwenda mapumziko matokeo yakiwa 2-1.
Algeria walipata bao la tatu katika dakika ya 53 lililofungwa na Carl Medjani akipokea pasi safi kutoka kwa Aissa Mandi.
Dakika ya 63, Kocha wa Tanzania, Salum Mayanga alifanya mabadiliko kwa kumtoa Ndemla na nafasi yake kuchukuliwa na Erasto Nyoni.
Mabadiliko mengine yalifanyika dakika ya 75 akitoka Shiza Kichuya na nafasi yake kuchukuliwa na Mohamed Issa, lakini mabadiliko hayo hayakuisaidia Stars.
Dakika ya 80, Algeria walifumania kwa mara nyingine nyavu za Tanzania kupitia kwa Baghadad Bounedjah akipokea pasi kutoka kwa Riyad Mahrez na kuwapiga chenga mabeki na kipa wa Stars na kufunga bao la nne kwa wenyeji.
Dakika ya 88 kocha Mayanga alimtoa Simon Msuva na nafasi yake kuchukuliwa na Rashid Mandawa. Mpaka mwisho wa mchezo Tanzania ililala kwa mabao 4-1 na timu hiyo inatarajiwa kurudi nchini wakati wowote kuanzia sasa kujiandaa na mechi dhidi ya DR Congo itakayochezwa Machi 27 jijini Dar es Salaam.
Na Vicent Segona vicent@spoti.co.tz
Chanzo: Mwanaspoti

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here