CAF yazisubirisha Simba, Yanga

0
4

MECHI ya marudiano ya Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu kati ya watani wa jadi nchini, Simba na Yanga sasa itafanyika Aprili 29, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, imeelezwa.

Awali mchezo huo ulipangwa kufanyika Aprili 7, mwaka huu, lakini sasa umesogezwa mbele kutokana na siku hiyo mabingwa watetezi Yanga kukabiliwa na mechi ya hatua ya mtoano ya Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya Welayta Dicha kutoka Ethiopia, unaosimamiwa na Shirikisho la Soka Afrika (Caf).
Katika mechi ya kwanza iliyofanyika Oktoba Mosi mwaka jana, timu hizo zinazodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, zilitoka sare ya bao 1-1.
Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Afisa Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Tanzania, Boniface Wambura, alisema kuwa ratiba hiyo inaweza kubadilika tena endapo Yanga itasonga mbele na pia imezingatia majukumu mengine ya klabu ambazo zinashiriki michuano ya Kombe la FA.
Wambura alisema kuwa hakuna timu ambayo haina changamoto, na kuzitaja baadhi ya mechi nyingine za “viporo” kuwa ni Njombe Mji itaikaribisha Simba Aprili 3, mwaka huu na vinara hao wataifuata Mtibwa Sugar kwenye Uwanja wa Jamhuri ifikapo Aprili 9, mwaka huu.
Alizitaja mechi nyingine ni kati ya Yanga dhidi ya Stand United itakayopigwa Aprili 11, wakati Simba dhidi ya Mbeya City itachezwa Aprili 12 na Tanzania Prisons watawafuata Wekundu wa Msimbazi Aprili 16 na baadaye vinara hao wataelekea Iringa kucheza na wenyeji wao Lipuli FC ifikapo Aprili 20, mwaka huu.
Mabingwa watetezi Yanga watasafiri kwenda Mbeya kuikabili Mbeya City Mei Mosi na watarejea Dar es Salaam kuwakaribisha Mbao FC Mei 5 huku Mei 6 Simba wakivaana na Ndanda FC kutoka Mtwara.
“Kiukweli ratiba hii imebana sana kwa timu zote na hasa zile ambazo zinashiriki Kombe la FA na Yanga wao wamebanwa zaidi kwa sababu bado wako katika mashindano ya kimataifa, na itabadilika tena kama watatinga hatua ya makundi na itazingatia kama ataanzia nyumbani au ugenini,” alisema Wambura.
Aliongeza kuwa mechi zote za ligi hiyo inayotarajiwa kumalizika Mei 26, mwaka huu, ikifuatiwa na mchezo wa Fainali ya Kombe la FA utakaopigwa Mei 31, mwaka huu, zimepangwa kwa kuzingatia kanuni ambayo inaeleza kuwa na tofauti ya saa 72 kati ya mechi moja na nyingine.
Source:IPP Media

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here