Azam yaitishia nyau Mtibwa Sugar

0
2

Azam FC imeichapa Friends Ranger mabao 5-0 katika mchezo wa kirafiki uliofanyika juzi kwenye Uwanja wa Azam Complex, ikiwa ni maandalizi ya mchezo wake wa robo fainali ya Kombe la Shirikisho dhidi ya Mtibwa Sugar.

Katika mchezo huo wenyeji Azam walianza vema baada ya kupata bao la kwanza dakika ya nne, lililofungwa na winga Enock Atta kwa mkwaju wa penalti baada ya Idd Kipagwile kuangushwa kwenye eneo la hatari.

Uzembe wa safu ya ulinzi ya Friends uliinufaisha tena Azam FC dakika ya 40 baada ya mshambuliaji Mbaraka Yusuph, kuipatia bao la pili na kufanya timu yake iende mapumziko ikiwa mbele kwa mabao mawili.

Dakika ya 67 , winga Joseph Kimwaga alichukua nafasi ya Mbaraka, ikiwa ni mechi yake ya kwanza msimu huu baada ya kupata majeraha ya goti wakati timu hiyo ikijiandaa kucheza mchezo wa kwanza wa ligi dhidi ya Ndanda mkoani Mtwara.

Dakika ya 73, kiungo Salmin Hoza, alitumia jitihada binafsi na kuipatia bao la tatu Azam FC kwa shuti la umbali wa takribani mita 30 lililomshinda kipa wa Friends Ndugu Juma.

Kimwaga aliingia na moto ukiwa ni mchezo wake wa kwanza, alihitimisha ushindi mnono wa Azam FC kwa kufunga mabao mawili dakika ya 75 na 82, ya mchezo huo.

Mara baada ya mchezo huo, kikosi cha Azam FC leo Jumatatu kinatarajia kurejea kukamilisha maandalizi ya kuikabili Mtibwa Sugar katika mchezo muhimu wa robo fainali ya michuano ya Kombe la Azam.

Chanzo: Habarileo

LEAVE A REPLY

Please enter your comment!
Please enter your name here