Young Africans yasalimu amri, yaomba radhi

1 week ago 77

Uongozi wa klabu ya Young Africans umethibitisha kupokea taarifa ya kutoruhusiwa kucheza bila mashabiki kwenye mchezo wa kesho wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya awali dhidi ya Rivers United ya Nigeria.

Young Africans watakuwa wenyeji wa mchezo huo, uliopangwa kupigwa mishale saa kumi na moja jioni, Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, na tayari walijiandaa kuwa na mashabiki uwanjani hapo.

Klabu hiyo kongwe katika ukanda wa Afrika Mashariki na Kati jana Ijumaa (Septemba 10), ilitangaza viingilio kupitia kurasa za mitandao ya kijamii ya Young Africans, lakini Shirikisho la soka nchini TFF, lilitoa ufafanuzi wa taarifa waliyoipokea kutoka CAF ambayo inapiga mafurufuku michezo ya awali kuwa na Mashabiki kwa kuhofia maambukizi ya Uviko 19 (Covid 19).

Kutokana na ufafanuzi huo Uongozi wa Young Africans nao ukathibitisha kupokea taarifa za marufuku hiyo na kuwaomba radhi Mashabiki na Wanachama wao ambao walikua wameshaanza maandalizi ya kwenda Uwanja wa Benjamin Mkapa kwa ajili ya kuishangilia timu yao.